INEQUALITIES

Makundi ya haki yaonya kuwa huduma ya afya ya kibinafsi inaathiri wengi, kufuja rasli mali za umma

Hatua ya serikali kuunga mkono upanuzi wa huduma ya afya ya kibinafsi nchini Kenya imesababisha kutengwa na kurudisha nyuma hatua za kutimiza malengo ya afya kwa wote, makundi mawili ya haki yamesema kwenye ripoti iliyotolewa leo. Sera za kitaifa zilizokusudiwa kuongeza ushiriki wa sekta ya kibinafsi katika utoaji wa huduma ya afya, pamoja na uwekezaji duni katika mfumo wa umma, zimechangia kuenea kwa wahudumu wa kibinafsi ambao mara nyingi hutoa huduma duni, hupuuza vipaumbele vya afya ya umma, na kuwasukuma wakenya wengi katika umasikini na malimbikizi ya madeni.

Ripoti hiyo ya kurasa 52, “Tiba Tatanishi: Athari ya ubinafsishaji wa Huduma ya Afya nchini Kenya,” imeandikwa na Hakijamii kwa pamoja na Kituo cha Haki za Kibinadamu na Haki za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha New York (CHRGJ). Ripoti hiyo inabaini kwamba ubinafsishaji umewekea watu binafsi na serikali mzigo mkubwa wa gharama, umewazuia watu wengi kupata huduma ya afya, na unahujumu haki ya afya. Sera kuu ya serikali ya kutimiza mpango wa afya kwa wote—mpango wa kupanua bima ya jamii inayoegemea sekta ya kibinafsi kupitia Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF)—unatishia kuzidisha matatizo haya.

“Ubinafsishaji si suluhisho tosha kwa kutimiza mpango wa afya kwa wote,” alisema Philip Alston, aliyekuwa Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na mwandishi mwenza wa ripoti hii. “Watetezi wa ubinafsishaji wa huduma ya afya hutoa ahadi za kila aina kuhusu jinsi hatua hiyo itapunguza gharama za matibabu na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya afya, lakini utafiti wetu umepata kwamba wahudumu wa kibinafsi wameshindwa kabisa kutimiza ahadi zao.”

“Watetezi wa huduma ya afya ya kibinafsi wameshindwa kutoa ufafanuzi halisi wa hali ilivyo,” alisema Nicholas Orago, Mkurugenzi Mtendaji wa Hakijamii na mwandishi mwenza wa ripoti hii. “Huku wengi wakihusisha huduma ya kibinafsi na vituo vya kiwango cha juu, ‘mabwanyenye’ na ‘wachochole’ hukumbana na aina tofauti za sekta ya kibinafsi. Huduma ya afya ya kibinafsi imekuwa na madhara makubwa kwa watu maskini na jamii zilizoko hatarini, ambazo hulazimika kutumia wahudumu nafuu wa kiwango cha chini, ambao hutoa huduma ambazo mara nyingi ni hatari au hata kinyume cha sheria.”

Ubinafsishaji umedhibitishwa kuwa wa gharama kubwa kwa watu binafsi na serikali. Sekta ya afya ya kibinafsi hutegemea zaidi ufadhili wa serikali, ikiwemo matumizi ya mabilioni ya pesa kila mwaka kutoa kandarasi kwa vituo vya kibinafsi, ruzuku kwa huduma ya kibinafsi, na malipo kwa miradi ya kisiri ya ushirikiano wa sekta za umma na kibinafsi. Watu binafsi hukabiliwa na ada za juu zaidi katika vituo vya kibinafsi, ambako matibabu wakati mwingine yanagharimu mara kumi na mbili zaidi ya gharama katika sekta ya umma.

“Huduma ya afya ni biashara kubwa, huku mashirika ya kimataifa na kampuni za ufadhili wa kibinafsi zikilenga kujinufaisha kutoka sekta hiyo nchini Kenya,” alisema Rebecca Riddell, Mkurugenzi mwenza wa mradi wa Haki za kibinadamu na  Ubinafsishaji katika kituo cha CHRGJ na mwandishi mwenza wa ripoti hii. “Kampuni hizi zinatarajia faida kutoka uwekezaji wao, hatua ambayo husababisha bei za juu zaidi katika sekta ya kibinafsi huku rasli mali haba za umma zikitumika kuimarisha faida za sekta ya kibinafsi.”

Ripoti hii imeandikwa kutokana na mahojiano yaliyofanyiwa watu zaidi ya mia moja themanini wakiwemo wagonjwa na watoaji wa huduma ya afya, maafisa wa serikali na wataalamu. Watafiti walizungumza na wanajamii kutoka mitaa ya mabanda katika miji ya Mombasa na Nairobi na vile vile maeneo ya mashambani katika kaunti ya Isiolo. Wengi walieleza jinsi walivyotengwa kutoka huduma ya kibinafsi au kukabiliwa na matatizo kugharamia matibabu, kama vile kulazimika kuuza mali muhimu kama shamba ama kukatiza masomo ya watoto na fursa nyingine za kutafuta riziki. Wengine walielezea matokeo ya kusikitisha ya huduma ya kiwango cha chini katika vituo vya kibinafsi, ikiwemo vifo ambavyo vingeepukika na ulemavu. Athari zake ni kubwa zaidi kwa watu maskini au wenye mapato ya chini, wanawake, walemavu, na wale wanaoishi sehemu za mashambani.

Watafiti pia walipata kwamba sekta ya kibinafsi nchini Kenya imejilimbikiza zaidi katika huduma zenye faida kubwa,na kupuuza maeneo yenye faida duni, wagonjwa, na huduma. Wafanyikazi wa huduma ya afya katika sekta ya kibinafsi walieleza jinsi walivyohitajika kutimiza “malengo” ya kuhudumia idadi fulani ya wagonjwa na vile vile kufanya kazi katika mazingira duni ikilinganishwa na sekta ya umma.

“Mkinzano kati ya faida na malengo ya afya ya umma unafaa kuwachochea watungaji sera kufikiria upya utegemeaji wa sekta ya kibinafsi,” alisema Bassam Khawaja, Mkurugenzi mwenza wa mradi wa Haki za kibinadamu na Ubinafsishaji na mwandishi mwenza wa ripoti hii. “Huduma nyingi muhimu za afya zina thamani kubwa au ni muhimu kwa kuokoa maisha licha ya kwamba hazina faida kubwa kibiashara.”

Mpango unaotarajiwa wa kusambaza kote nchini huduma ya bima ya afya ya lazima utachangia kuelekezwa kwa pesa zaidi za umma kwa wahudumu wa kibinafsi bila kusitisha kutengwa na gharama za juu. Ingawa NHIF inatoa bima ya umma, hazina hiyo hutoa kandarasi nyingi kwa vituo vya kibinafsi, hulipa wahudumu wa kibinafsi kwa viwango vya juu, na hulipa kiwango kikubwa  cha madai kwa wahudumu wa kibinafsi. “Kupanua huduma kupitia NHIF badala ya kuwekeza katika mfumo dhabiti wa huduma ya afya ya umma ni hatua kubwa kurudi nyuma,” Orago alisema.

Msukumo mkubwa wa ubinafsishaji umetoka kwa washirika wa kigeni. Washirika wakuu wa maendeleo wamehimiza Serikali ya Kenya kuongeza jukumu la sekta ya kibinafsi katika utoaji wa huduma ya afya, ikiwemo  mashirika ya kifedha ya kimataifa, wakfu za kibinafsi, na mataifa tajiri yanayotafuta masoko mapya kwa bidhaa zao.

“Dhamira ya kiitikadi kwa sekta ya kibinafsi imekiuka haki za wakenya, huku washirika wa maendeleo wakieneza na kufadhili huduma ya kibinafsi bila kuwajibika,” Alston alisema. “Usiri mkubwa juu ya makubaliano mengi na sekta ya afya ya kibinafsi unatoa mwanya kwa ufisadi na maslahi ya kibinafsi.”

Ripoti hii inabainisha kwamba serikali inapaswa kufikiria upya msaada wake kwa sekta ya kibinafsi na kutoa kipaumbele kwa mfumo wa huduma ya afya ya umma, ambao bado unatoa huduma nyingi kwa wagonjwa wanaoruhusiwa kwenda nyumba na wale wa kulazwa nchini Kenya licha ya uhaba wa fedha. “Ingawa serikali inafaa kushughulikia mapungufu makubwa katika mfumo wa afya wa umma, uwekezaji maarufu wa hivi karibuni unaonyesha hamu kubwa ya matumizi ya huduma ya afya ya umma,” alisema Alston.

“Kukiwepo na nia njema ya kisiasa na rasli mali, mfumo wa huduma ya afya wa umma una nafasi bora kutoa kwa wakenya wote huduma iliyo rahisi kupatikana, yenye gharama nafuu, na ya kiwango cha juu ambao wanastahili kupata,” alisema Orago.

This post was originally published as a press release on November 16, 2021.